Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA – ZNZ), Dkt. Mzuri Issa amewataka wataalam Sekta ya Afya kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waandishi wa Habari katika kutoa taarifa sahihi za afya ya uzazi kwa jamii na Vijana waweze kujikinga na madhara yanayoweza kuwapata.

Dkt. Mzuri ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Habari na Wataalam wa Afya wenye lengo la kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi wa utetezi wa masuala ya afya ya uzazi kwa kutumia Vyombo vya Habari.

Amesema, ili kufikisha elimu sahihi ni lazima kuweka na kuripoti takwimu za masuala haya, ikiwemo vifo vya mama na watoto, mimba za utotoni na kwamba utoaji wa elimu ya mnyambuliko wa umri wa kubeba mimba pamoja na athari zinazoweza kutokea kulingana na umri husika ni elimu muhimu inayohitajika kwa vijana.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA – ZNZ), Mzuri Issa.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA – ZNZ, Abdulrahman Mohammed alisema la mradi huo ni kuongeza uelewa kupitia Vyombo vya Habari kuhusu masuala ya haki ya afya ya uzazi kwa Wanawake na wasichana, ili kuwasaidia kuepuka na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.

Naye, Afisa Msimamaizi wa Mradi huo, Zaina Mzee alisema wamewajengea uwezo Waandishi wa Habari kuifahamu elimu hiyo na kuwasaidia kuandaa vipindi, na habari za uchambuzi kupitia Vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii, juu ya mabadiliko ya tabia na afya ya uzazi kiujumla.

Alisema, “mradi ulianza na utafiti ambao uligundua kuwa waandishi wengi hawana uelewa juu ya masuala ya afya ya uzazi, hivyo tukaandaa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo na sasa wanaripoti vizuri habari hizi na wanaisaidia jamii kupata huduma stahiki.”

Wadau wa Habari na Wataalam wa Afya waliokutana kujadili masuala ya haki ya afya ya uzazi na maendeleo ya mradi.

Amina Hussein, Daktari Dhamana Wilaya ya Kati Unguja alipongeza Waandishi wa Habari kwa uthubutu wa kuibua changamoto mbalimbali ambazo tayari zimepatiwa ufumbuzi na kuwaomba kuendelea kuielimisha jamii na kutoa taarifa ambazo zinasaidia jamii kuondokana na changamoto.

Awali, Mwandishi wa Habari mkongwe Zanzibar, Salim Said aliwaomba wataalam wa afya kuwa wepesi wa kutoa mashirikiano kwa kutoa taarifa na takwimu pindi zinapotakiwa na waandishi wa habari ili kuwezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mradi wa kuendeleza utetezi wa vyombo vya habari juu masuala ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana wa mjini na vijijini ,ni mradi wa mwaka mmoja ambao  unatekelezwa kwa mashiriano na TAMWA ZNZ pamoja na  shirika la WELLSPRING.

Miguel Gamondi atambia kikosi chake
Sakata la Mwakinyo: TPBRC yashauriwa la kufanya