Wataalamu wa afya nchini, wametakiwa kutimiza wajibu katika utendaji wa wa kazi ili kuboresha huduma kwa wananchi na kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Afya, ikiwemo kusimamia fedha za wadau na za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kuokoa vifo vinavyozuilika.
Wito huo, umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi katika kikao chake na Waganga Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na Wafawidhi kilichofanyika kwa njia ya mtandao kikiwashirikisha Wakurugenzi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Wizara ya Afya.
Amesema, “Wizara imejipanga kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ‘clinical audit’ katika ngazi ya utoaji huduma kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya, ili kuboresha huduma na kuleta matokeo kwa wananchi.”
Prof. Makubi, pia amewataka Wataalamu wa afya kufuata misingi, miongozo na taaluma zao wakati wa utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya lugha kwa wananchi wahitaji wa huduma ili kuondosha malalamiko yasiyo na ulazima.
“Suala la lugha mbaya kwa wananchi wanapoenda kupata huduma, hii ni lazima muifanyie kazi, lakini pia tujitahidi kusimamia huduma za mama na mtoto katika maeneo yao na kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito.” amefafanua Prof. Makubi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afya OR-TAMISEMI Dkt. Grace Magembe alisema bajeti ya TAMISEMI ya mwaka 2022/2023 imeweka kipaumbele kwenye vifaa tiba, utumishi, kujenga na kukarabati hospitali mpya za Wilaya na Zahanati ili kuboresha huduma kwa wananchi.