Kongamano la kimataifa la wataalam wa kifua kikuu (TB), limefanyika jijini Nairobi nchini Kenya kujadili mbinu za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma, kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huo wa Kifua kikuu, husambazwa kupitia hewa pale mtu anapovuta iliyo na bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis wakati wa kukohoa na kwa mujibi wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, TB ni moja ya magonjwa 10 yanayosababisha vifo vingi duniani.
Aidha, inaarifiwa kuwa, kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa kifua kikuu huathiri mapafu, lakini sehemu nyengine mwilini pia zinaweza kuambukizwa huku takwimu za WHO zikionesha kuwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani ni watu wazima, wengi wakiwa ni Wanaume.
Shirika la WHO, limeiondoa Kenya na mataifa mengine 5 kwenye orodha ya mataifa 30 yaliyo na visa vingi vya wagonjwa wa kifua kikuu duniani huku taarifa yake ya mwaka wa 2022 ikielezea kuwa kwa mataifa mengine, hali ilikuwa mbaya zaidi ukizingatia athari za janga la corona au COVID-19.
Afisa wa matibabu na msimamizi wa mpango wa kifua kikuu kwenye kaunti ya Nairobi, Mary Nzamalu amesema, ”Kwa sasa wagonjwa wakija wanapimwa Uviko-19 na kifua kikuu kwa pamoja maana dalili zinafanana.”
Hata hivyo, amesema idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo imeongezeka kutokana na waliokuwa hawawezi kufika hospitalini kwasababu ya vikwazo vya Uviko-19 kuwa na uhuru wa kutembea na kunapata huduma.