Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Madaktari nchini Kenya (KEMRI), wamegundua aina mpya ya mbu kutoka bara la Asia upande wa Kusini, ambaye anastahimili viua wadudu vinavyotumiwa barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Kemri, Dkt Samuel Kariuki amesema walimtambua mbu huyo, Anopheles stephensi, wakati wa ufuatiliaji wa kawaida katika kaunti ya Marsabit kaskazini.
Amesema, takwimu kutoka hospitalini pia zilionyesha ongezeko la visa vya malaria, ingawa haukuwa msimu wa kawaida wa ugonjwa huo, kutokana na mbu wa kienyeji kutofanya vizuri katika maeneo kavu.
Mbu huyo vamizi, anaweza kustawi katika misimu ya kiangazi na ya mvua na anaweza kuzaliana popote. Katika nchi nyingine, mabuu yake yamepatikana katika vyombo vya maji katika maeneo ya mijini.
Aidha, Dkt. Kariuki amesema wana wasiwasi kuwa maambukizi ya malaria yataendelea kwa mwaka mzima badala ya kuwa ya msimu hasa katika maeneo ya mijini.
Hata hivyo, Watafiti hao wanawataka Wananchi kutumia zana zilizopo kudhibiti malaria kama vile kulala kwenye vyandarua vilivyotiwa dawa, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuvaa nguo za mikono mirefu ili kuzuia kuumwa na mbu.