Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa Watafiti kufanya tafiti zitakazosaidia kupata ufumbuzi wa changamoto za kimazingira hususan mabadiliko ya tabianchi.
Jafo ametoa rai hiyo wakati akizindua Programu ya Utafiti kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) leo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam ambapo katika hafla hiyo Tanzania imenufaika na zaidi ya shilingi bilioni 9 zilizotolewa na Serikali ya Norway kupitia Shirika la Maendeleo la NORAD kwa ajili ya kufanya utafiti huo.
Amesema, uchumi unaweza ukaathirika kutokana na changamoto za kimazingira ambapo jamii hushindwa kufanya shughuli za kujipatia kipato ikiwemo kilimo na ufugaji kutokana na ukame na kwamba katika kukabiliana na changamoto hiyo watafiti wanatarajiwa kutoa majawabu kuhusu sekta gani itasaidia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Maeneo haya tuna kazi kubwa ya kujua ni tafiti zipi kwa mfano kama ni kilimo gani kinaweza kufanyika katika maeneo yanayokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ninyi watafiti mna jukumu kubwa la kutusaidia katika hili,” amesema.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Bodi ya COSTECH Prof. Makenya Maboko pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungua wamesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na ushirkiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.