Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema watafiti wanatakiwa kuwa msaada kwa kutafsiri matokeo ya tafiti zao ikiwemo kuchapisha matokeo hayo sambamba na mapendekezo ili kuboresha maeneo ya tafiti hizo kwa lugha nyepesi kama moja ya sehemu ya vivutiuo vya Utalii.
Othman ameyasema hayo hii leo leo Agosti 9, 2022 wakati akifungua Kongamano la 16 la kimataifa la Jumuiya ya wanazuoni na watafiti wa Mambo ya Kale, linalofanyika katika ukumbi wa SUZA Maruhubi, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi.
Amesema, ushirikiano baina ya Wataalamu na Watafiti mbali mbali unahitajika, hasa katika nyanja ya mafunzo na Teknolojia, maabara, vifaa pamoja na machapisho ili kuendeleza vyema kazi hiyo na kufikia malengo.
“Taaluma ya Mambo ya Kale na Urithi wa Utamaduni unagusa sekta zote za kiuchumi, Kijamii , kisiasa, Teknolojia, Mazingira na Magonjwa mbali mbali, na hili ni tegemeo la taifa kuweza kufahamu nchi ilikotoka, ilipo sasa na inakokwenda, tafiti ni mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo yanayopangwa nchini,” amesema.
Aidha, Makamu wa Rais huyo amewakaribisha watafiti mbali mbali duniani kuja Zanzibar kutafiti masuala ya akiolojia ya baharini kwa kuzingatia sera ya Serikali ya awamu ya nane ya Uchumi wa Bluu na kwamba utajiri wa Urithi uliopo baharini unaweza kutumika kama fursa muhimu ya kukuza sekta hiyo.
Amefafanua kuwa, “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa kipaumbele katika masuala ya Utafiti wa namna hiyo na ndio maana imeunda wizara kamili inayoshughulikia mambo ya Kale na kwamba ni fursa kwa wataalamu kufanya tafiti mbali mbali za aina hiyo hapa Zanzibar.”
Awali, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Simai Mohammed Said amesema Serikali kupitia wizara yake ipo tayari kutoa ushirikianao utakayohitajika katika kufanikisha tafiti mbali mbali zinazohusu mambo ya Kale Zanzibar.
Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki mbali mbali kutoka nje ya Tanzania wakiwemo Kenya, Unganda, Zimbabwe, Aljeria, Ethipia, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, DRC Congo, Senegle, Najeria, Mali, Moroco na Wenyeji Tanzania na Zanzibar.