Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Nchini Tanzania (TEA), Dkt. Erasmus Kipesha ameweka wazi fursa na faida kubwa kwa Watu binafsi ama Taasisi ambazo zitashiriki kuchangia Mfuko wa Taifa wa Elimu nchini kupitia mamlaka hiyo.
Akizungumza kwenye kikao kazi maalum na Wanahabari leo Novemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam, Dkt. Kipesha chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, amesema;
“Ukichangia elimu kupitia Mfuko wa Elimu tutakupa cheti ambacho unaweza kukipeleka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ukapata nafuu ya kodi.
“Lakini, pia ukichangia Mfuko wa Elimu tutakutangaza na kukuingiza katika regista maalum.Kwa hiyo mkija kuchangia elimu kupitia Mfuko wa Elimu kuna manufaa mengi mno. Kwahiyo kama unapenda kusaidia Elimu ama Watoto wasio na uwezo Kielimu unaweza kupotia njia hii ya TEA”
Amefafanua kuwa, cheti ambacho mchangiaji huwa anapatiwa kinakuwa kimesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kinaweza kutumika ndani ya miaka mitatu kwaajili ya msamaha wa Kodi.
“Ndani ya miaka mitatu cheti hicho kitakuwa kime-expire. Kinacho-expire ni ile nafuu ya kodi, lakini cheti chako hakitakufa, kitakuwa hai siku zote.”
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa.Amesema, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013, madhumuni yake ikiwa ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharimia miradi ya elimu ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa, katika ngazi zote za Elimu kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.
Kuuanzia mwezi Oktoba 2017, mamlaka pia ilipewa jukumu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia la kusimamia na kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund-SDF).Mfuko wa SDF ulikuwa unatoa ufadhili wa mafunzo ya kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele zinazoratibiwa na Programu ya ESPJ.
Kuhusu vyanzo vya mapato, Dkt.Kipesha amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya Mwaka 2001, Sura ya 412 pamoja na marekebisho yake ya Mwaka 2013, vyanzo vya mapato vya TEA ni pamoja na tengeo la kibajeti kwa ajili ya uendeshaji na miradi ya maendeleo. Vingine ni tozo ya asilimia 2.5 ya ushuru wa forodha wa huduma za mawasiliano ya kielektroniki. Kiwango kisichopungua asilimia 2 ya Bajeti ya Serikali ukitoa deni la Taifa.
Akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo, Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema, vikao hivyo vimelenga kuongeza uelewa wa kutosha kuhusu taasisi na mashirika hayo ya UMMA.