Wakazi wa vijiji vya Kazania Wilaya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma na Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoro wametakiwa kutunza na kuendeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini (EBARR) ili kukabiliana na ukame.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama alipofanya ziara na kukagua miradi ya kilimo cha mbogamboga kupitia kitalu nyumba, ufugaji wa nyuki na ujenzi wa kisima katika vijiji hivyo inayotekelezwa na EBARR kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amewataka wakazi hao kuwa wamoja kwa kuepuka majungu na fitina hasa katika kipindi cha sasa walichoanza kupata kipato kutokana na uzalishaji wanaoufanya.
Dkt. Mkama amesema kwenye miradi ya kujipatia fedha kwa wananchi wenye ushirikiano kumekuwepo na sintofahamu hali inayosababisha fitina na majungu hivyo kukosekana kwa amani.
“Ndugu zangu nawaomba msiruhusu kabisa kutokea kwa hali hii na endapo kutatokea malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya fedha mntakiwa kufanya uchunguzi na sio kukurupuka kutoa maamuzi kwa kuwa kwenye wengi kuna mengi,“ amesema.