Serikali ya Tanzania inathamini mchango mkubwa unaotolewa na Serikali ya Japani kupitia Shirika  la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA)   ambalo limekuwa likishirikiana na Serikali katika kazi mbalimbali  za maendeleo hapa nchini.

Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Bi. Susan Mlawi  alisema hayo mapema leo katika ukumbi wa mikutano wa Utumishi wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha watalaam wa kujitolea kutoka Japani.

“Tangu mwaka 1967 hadi sasa zaidi ya vijana wa Japani 1,500  wameshafika  nchini na kufanya  kazi za kujitolea katika maeneo mbalimbali hata katika mazingira magumu” Bi. Mlawi alisema na kuongeza kuwa  kunufaika huko kwa Tanzania kunatokana na ushirikano baina ya Serikali ya Japani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano huo  na Japani  ili kuendelea kunufaika  hasa katika suala zima la kujengewa uwezo katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii , sekta ambazo pia  zimepewa kipaumbele  katika Awamu ya Pili ya  Mpango wa Serikali wa  miaka Mitano (5) wa Maendeleo inayoanza mwaka 2016/17 na kumalizika mwaka 2021 /22.

Kwa upande wake,  mwakilishi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Japani (JICA) nchini  Tanzania  Bw. Toshio Nagase  alisema wataalam hao ambao wako sita (6)  watafanyakazi ya kujitolea katika sekta ya elimu kwa miaka miwili na kwa kipindi hicho wanaamini Watanzania watakuwa wamenufaika na ujuzi toka kwa vijana hao.

Alisema watajitolea kufundisha masomo ya Sayansi, Hisabati, Masuala ya Maendeleo ya Jamii  na Michezo  katika shule za Sekondari , Shule za Msingi  na Ofisi za  Maendeleo ya Jamii katika Mikoa ya Morogoro, Pwani , Mtwara , Dodoma na Dar es salaam

Kanumba Star Search Yazinduliwa
Video: BASATA yawatahadharisha wasanii kusoma alama za nyakati, kufuata sheria