Serikali ya Zanzibar imesema inashirikiana kwa karibu na ubalozi wa Ukraine uliopo nchini Kenya kuangalia ni namna gani itawasafirisha watalii wa Ukraine wapatao elfu moja ambao hivi sasa wamekwama kisiwani humo baada ya kuzuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.

Leila Mohammed Musa, ambaye ni Waziri wa Utalii wa Zanzibar ameiambia BBC kwamba, watalii hao, tayari wanaendelea kupewa huduma za kibinadamu licha ya wengine kuwa wamemaliza siku zao za kutalii.

Amesema mpango uliopo ni watalii hao kupelekwa nchi jirani ya Poland. Hata hivyo, taarifa zaidi za kufanyika kwa zoezi hilo zitatolewa pindi Balozi wa Ukraine atakapofika kutoka nchini Kenya na kufanya mazungumzo na serikali ya Zanzibar hii leo.

Baadhi ya hoteli zimelazimika aidha kupunguza viwango vyao vya bei huku nyingine zikiamua kutoa hifadhi kwa wageni hao kwa malipo madogo.

Mmoja wa watalii hao, ambaye amekuja kutembea na mama yake, ameiambia BBC kwamba, hivi sasa wana wasiwasi iwapo wataweza kurudi nyumbani kwa wakati na iwapo watamkuta bibi yao mwenye umri wa miaka 84 akiwa katika hali nzuri.

Ukraine ilifunga anga yake kwa ndege za kiraia kufuatia mashambulizi kutoka Urusi, hivyo ndege zote za abiria kulazimika kusitisha safari zake.

Zanzibar, kwa miaka mingi, imekuwa ni kivutio kwa watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.

chanzo@bbc swahili

Jux kugawa Kitita kwa shabiki
Dkt.Mwinyi:Magonjwa adimu yanahitaji juhudi za pamoja kuyakabili