Watu watano wameuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini, baada ya kutokea vurugu kati ya magenge hasimu ya uchimbaji haramu wa madini.
Taarifa ya Polisi nchini humo, imesema miili mitano inayoaminiwa kuwa ya wachimbaji haramu ilipatikana karibu na shimo la kuingia mgodini, eneo lenye mabanda lijulikanalo kama Riverlea la magharibi mwa jiji la Johannerburg.
Hata hivyo, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa makundi mawili hasimu ya wachimbaji haramu yalikuwa yanafyatuliana risasi katika eneo hilo wakigombea umiliki wa mawe yaliyopatikana na machimbo.
Tukio hilo linatokea huku kukiwa na kiwango cha ukosefu wa ajira cha asilimia 32 nchini Afrika Kusini ambayo ina maelfu ya wachimbaji haramu waliopewa jina la utani la “zama zamas”, ambalo ni neno la Kizulu linalomaanisha “wale wanaojaribu.”