Watanzania wametakiwa kutosafiri kuelekea nchi jirani ya Msumbiji, bila kuwa na vibali au nyaraka halali zitazowatambulisha utaifa wao, na kutumia vivuko rasmi vinavyotambulika ili kuepuka madhara ya kiusalama yanayoweza kujitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa, amekanusha taarifa zinazodai kuwepo kwa raia wa Msumbiji wanaokimbilia katika maeneo ya jirani na mpaka wa Tanzania na wengine kushambuliwa.

Byakanwa amesema kuwa suala la kuwataka kutumia utaratibu huo linalenga kuimarisha ulinzi wa mipaka na kuendelea kujiridhisha juu ya kumbukumbu sahihi ya watanzania waliotoka na kuingia nchini.

Amesema kuwa kutokana na kukauka kwa maji katika mto Ruvuma, mpaka wa Tanzania na msumbiji unapitika kwa urahisi hata kwa kutembea na miguu.

Hata hivyo Byakanwa amekanusha uwepo wa taarifa kuwa machafuko yanayoendelea Msumbiji yameiathiri Tanzania, na kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimejipanga imara kulinda usalama wa mipaka yake.

Ronaldo aweka rekodi mpya Ureno
Rweyemamu: Hatutaidharau Mtibwa Sugar