Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kupunguza matumizi ya pombe kutokana na kuongezeka kwa tatizo la magonjwa yasiyoambukiza, huku takwimu zikionesha Tanzania ni ya tatu Barani Afrika kwa matumizi ya Pombe, ikifuatiwa na Shelisheli huku Uganda ikiongoza.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akizindua Kampeni ya kuelimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza kuwa ugonjwa wa Saratani ulianza kuongezeka kwa kasi mwaka 2020 ukionesha vifo vipya zaidi ya elfu 40, Saratani ya Mlango wa Kizazi ikishika namba moja.
Amesema, “hatusemi msinywe pombe, lakini tunasema mpunguze unywaji wa pombe kupita kiasi, takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha Tanzania Watu kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea kwa mwaka tunakunywa Lita 10.4 za pombe, kiasi cha pombe kinachonywewa Nchi nzima.
Aidha, amefafanua kuwa “kiasi hiki kikagawanywa kwa idadi ya Watanzania miaka 15 na kuendelea kila Mtu Mwanangu ni sawasawa tunatandika kwa mwezi Lita 1 kwa mwaka Lita 10.4, tupo nafasi ya tatu Afrika baada ya Uganda anafuata Shelisheli halafu sisi.”