Vijana 99 kati ya vijana 100 waliokuwa wanapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Kimataifa cha mafunzo ya Kilimo cha Arava kilichopo Kusini mwa Israel, wamehitimu mafunzo na kutunukiwa vyeti katika mahafali yaliyofanyika tarehe 12 Juni 2023 (The Arava International Center for Agriculture Training – AICAT.
Kupitia hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua aliwapongeza wahitimu wote na kuwaasa kuwa chachu ya mabadiliko wanaporejea nchini kwao kwa kufanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata nchini Israel.
Katika mahafali hayo, mradi mmoja kutoka kwa vijana wa Tanzania ulishinda tuzo ya Dola za Marekani 6,000.00 kutoka kwa The Dean Family Fellowship Grant, kufuatia shindano la kuandika na kuwasilisha mradi ambao vijana husika watafanya na kuleta mabadiliko chanya kwao na kwa jamii inayowazunguka, mara baada ya kurejea nyumbani.
Tuzo hii itawawezesha vijana walioshinda kuanzisha mradi husika na hivyo kujikwamua kiuchumi. Shindano lilihusisha nchi 12 ambazo zinashiriki mafunzo hayo na tuzo ilitolewa kwa nchi 7 ikiwemo Tanzania ambapo katika kundi hilo, mmoja wa washiriki alirejeshwa nchini kutokana na changamoto za kiafya.
Aidha, vijana 5 kutoka Tanzania walipata tuzo ya wanafunzi bora na kijana mmoja ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Tanzania amepewa ofa ya kuendelea na mafunzo kwa mwaka ujao wa masomo kutokana na nidhamu na uongozi uliotukuka.
Kwa mwaka wa masomo 2022/2023, Tanzania ilipewa nafasi za masomo 250 ambapo vijana 100 walipelekwa kwenye kituo cha AICAT na 150 walipelekwa kituo cha mafunzo cha Agrostudies ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo hayo kwa vijana wa Tanzania tangu programu hii ilivyoanza. Vijana wengine 150 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo yao mwezi Agosti 2023.
Kwa mwaka wa masomo 2023/2024, Tanzania imepewa nafasi 260 ambapo vijana 150 watapelekwa Agrostudies na vijana 110 watapelekwa AICAT ambapo Mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini hususan vijana hawa wanapofanyia kazi yale waliyojifunza.