Serikali imesema haitasita kumchukulia hatua mganga mkuu wa mkoa au wilaya atakayebainika kushindwa kusimamia fedha za Mradi wa Boresha Macho unaogharimu Shilingi za kitanzania Bilioni 6 na kutoa huduma za macho kwa watu 150,000 huku kati yao 13,500 watakaobainika na mtoto wa jicho watafanyiwa upasuaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Dokta Ntuli Kapologwe wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Boresha Macho unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID).

“Tuchukue mradi huu kama mtoto wetu na malengo tuliyoweka lazima yafanikiwe, hatutamvumilia mtu yeyote aidha anatoka shirika lisilo la kiserikali au serikalini ambaye hatatekeleza inavyotakiwa, kwasababu hizi fedha zimeletwa kwa ajili ya watanzania na wanapaswa kunufaika na kila uwekezaji unaofanywa kwenye macho,” amesema Dkt.Kapologwe.

Dokta Kapologwe amesema serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi ambapo zimeshuka hadi ngazi za kijiji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya anayeshughulia magonjwa yasiyo ambukiza, Dokta James Kiologwe, amesema asilimia moja ya watanzania wanakabiliwa na tatizo la uoni hafifu ambao husababisha kupata upofu.

Hata hivyo, amesema asilimia 75 ya matatizo yanayosababisha upofu yanazuilika na Wizara ya Afya inajivunia kufanya kazi na wadau kuhakikisha idadi hiyo ya watu wanapata tiba ili wasipate upofu.

Mradi huo utafikia halmashauri tano kati ya tisa za Mkoa wa Morogoro na kwa Mkoa wa Singida Halmashauri zote tisa zitanufaika.

Young Africans yaifuata Mtibwa Sugar kwa matumaini
TAKUKURU yakanusha kubambikiza kesi