Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu wawili kwa kosa la kujitambulisha kama kwa watu mbalimbali kama watumishi wa idara ya usalama wa taifa na kujihusisha na makosa ya kitapeli.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne, imeeleza kuwa Desemba 5, 2020 majira ya saa 11 jioni katika maeneo ya Kamanga, Wilaya ya Sengerema, jeshi la polisi liliwakamata watuhumiwa hao wawili waliokuwa wakijitambulisha kwa watu mbalimbali kuwa wao ni watumishi wa serikali idara ya usalama wa taifa kitengo cha afisa Kipenyo.

Baada ya mahojiano ya kina, watuhumiwa hao Severine Edward Mayunga mwenye umri wa miaka , mkazi wa kishiri ambaye amekutwa na kitambulisho kilichoandikwa “Severine Edward Mayunga, Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Idara ya Usalama wa Taifa, Kitengo cha Kikosi Maalumu Code Mt 82863, Nafasi Under Cover” na Abel Shiwa Mboja mwenye umri wa miaka 46, mkazi wa Kishiri wamekiri kuhusika  na makosa ya kitapeli na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu .

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa zinazohusu wahalifu na uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa haraka na watuhumiwa waweze kukamatwa kabla hawajatenda makosa .

Aidha,  katika tukio lingine polisi Mkoani humo inamshikilia Hamisi Omary (19), kwa tuhuma za mauaji ya  Vicent Renatus (17), Mwanafuzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Katunguru, mkazi wa mtaa wa msumbiji, aliyekutwa ameuawa katika chumba alichokuwa akiishi, mwili wake ukiwa na majeraha shingoni na kuporwa vitu mbalimbali vya nyumbani ikiwemo Televisioni na radio ‘sub woofer.”

Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kuhusika na mauaji  ya mwanafunzi huyo na kuwaonesha askari vitu vilivyoporwa kwa marehemu na kwenda kuviuza kwa Erasto Jackson mwenye miaka 22, mkazi wa Kitangiri Mkoani humo ambaye naye amekamatwa na kuhojiwa kwa tuhuma za kuwa mhalifu sugu wa kupokea mali za wizi.

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wengine wa tukio hilo.

Kesi ya Mwana FA, AY yatenguliwa
'Mo' atoa somo zito Simba SC

Comments

comments