Wachezaji Joash Onyango, Taddeo Lwanga na Mzamiru Yassin huenda wakaukosa mchezo wa Robo Fainali wa michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Dodoma Jiji FC, utakaochezwa kesho Jumatano (Mei 26), kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Wachezjai hao watatu wapo kwenye hatihati hiyo, kufuatia majeraha walioyapata kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

Kuhusu wachezaji ambao watakosekana kesho, Meneja wa timu ya Simba SC Patrick Rweyemamu, amesema kuwa mazoezi ya leo jioni yatatoa muelekeo wa nani atakosekana na nani atakuwepo, kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Lwanga na Onyango hawa waligongana katika harakati za kuokoa hatari huku Mzamiru yeye alishindwa kumaliza mchezo huo kutokana na maumivu aliyopata.

Mshindi wa mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Dodoma Jiji FC atakutana na mshindi wa mchezo wa Mei 26 kati ya Rhino Rangers na Azam FC utakaochezwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

TFF yathibitisha timu nne kimataifa
Wizara ya Mambo ya Ndani yavalia njuga kukomesha uhalifu