Imefahamika kuwa Uongozi Mbeya City umeachana na viongozi watatu wa benchi la ufundi huku sababu zikiendelea kufanya kuwa siri klabuni hapo.
Mbeya City inayohaha kusaka matokeo mazuri kwa sasa, inajindaa na michezo miwili ya mwisho dhidi ya Yanga na KMC FC kusubiri hatma yao ya kubaki au kushuka daraja.
Taarifa kutoka jijini Mbeya zinaeleza kuwa kocha msaidizi, Anthony Mwamlima, kocha wa makipa, Ally Mustafa ‘Bartez’ na daktari wao Omary Stanley wote wametimuliwa kazi huku sababu zikiwa hazijulikani.
Aliyekuwa daktari wa timu hiyo, Stanley amethibitisha kutokuwa kikosini tangu City ilipokuwa ikijiandaa na mchezo wake dhidi ya Geita Gold akifafanua walifikia makubaliano na mabosi wa timu hiyo.
Kocha msaidizi, Mwamlima amekiri “Mkataba wangu ulikuwa wa kila mwaka lakini hadi safari ya Geita sikuwepo kikosini licha ya maandalizi yote kushiriki hivyo niliitwa na uongozi tukapeana mkono wa kwa kheri”
“Nadhani ni ishu ya mtu binafsi kuamua kushawishi uongozi kutuacha, mkataba wangu ulikuwa uishe mwishoni mwa msimu huu ila waliamua kuvunja hivyo kwa sasa nipo nyumbani nasubiri sehemu nyingine itakayonihitaji,” amesema Stanley aliyewahi kuhudumu Mbeya Kwanza
Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Emanuel Kimbe amesema; “Hakuna kitu kama hicho, timu imefika usiku wa kuamkia jana Jumanne (Mei 16) na tunaendelea na mipango mikakati ya kujiandaa tena na mechi hizi zilizobaki,”