Polisi nchini Nigeria, imesema kundi la watu waliokuwa na silaha wamewateka nyara watawa wanne wa Kikatoliki katika jimbo la Imo, kusini mashariki mwa Nigeria, ambako utekaji nyara kwa ajili ya fidia umeenea,
Msemaji wa Polisi wa Imo, Michael Abattam amesema watawa hao walitekwa nyara siku ya Jumapili Agosti 21, 2022 karibu na mji wa Okigwe wakiwa njiani kuelekea kwenye misa ambapo mpaka sasa haijulikani eneo walilopelekwa na bado wanafuatilia.
“Tuko katika msururu wa watekaji nyara ili kuwakomboa waathiriwa, watekaji wanawachukua watu na kudai fidia hii ni hali isiyokubalika katika maisha yetu na tutalazimika kukomesha mipango kama hii Polisi ipo imara na tutawakamata wahusika,” alisema Abbatam.
Hakuna kundi lolote ambalo hadi sasa lililodai kuhusika na utekaji nyara huo, ambapo kwasasa unachukuliwa kuwa ni jambo la kawaida katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambayo imekumbwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi na kuandamwa na uhalifu ulioenea.
Ingawa mateka wengine huuawa, wengi huachiliwa baada ya kulipwa fidia ambapo katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa dini wamekuwa wakilengwa zaidi na wahalifu, si kwa sababu za kidini au kiitikadi, bali ni kwa sababu Kanisa linaonekana kuwa na uwezo wa kuhamasisha waamini kulipa fidia.
Kusini-mashariki mwa Nigeria pia inakabiliwa na ongezeko la ghasia zinazohusishwa na Vuguvugu Huru la Watu Wenyeji wa Biafra (Ipob), na kundi la Ipob, ambalo linatafuta taifa tofauti kwa ajili ya kabila la Igbo, limekanusha mara kwa mara kuhusika na ghasia katika eneo hilo.