Polisi nchini Nigeria imesema, kundi la watu wenye silaha waliokuwa wamewateka watawa wanne Agosti 21, 2022 wa Kanisa la Katoliki jimboni Imo lililopo eneo la kusini mashariki, wamewaachilia huru watumishi hao wa Mungu bila masharti.
Msemaji wa Polisi wa jimbo la Imo, Michael Abattam amesema Watawa hao wanne, waliotekwa nyara karibu na mji wa Okigwe katika Jimbo la Imo, waliachiliwa siku ya Jumanne Agosti 23, 2022 na hawajakutwa na madhara na haikufahamika mara moja ikiwa walilipa ili kuweza kuachiliwa.
Matukio ya utekaji nyara, ni jambo la kawaida katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambayo imekumbwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi na kuandamwa na uhalifu ulioenea maeneo mengi hasa katika ukanda wa Mashariki.
Ingawa mateka wengine huuawa, wengi huachiliwa baada ya kulipwa fidia na katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa dini wamekuwa wakilengwa zaidi na wahalifu, si kwa sababu za kidini au kiitikadi, bali ni kutokana na uwezo wa kuhamasisha waumini kuchanga na kulipa fidia.