Bodi ya Bima ya Amana (DIB), imetangaza kuanza kuwalipa wateja wa benki tano zilizofutiwa leseni mwishoni mwa mwezi huu, na imeeleza kuwa malipo hayo yataanza kufanyika Machi 28 mwaka huu kwa watejaa wote wa benki ya wananchi Njombe, Meru, Ushirika Kagera, Covenant na Ephata.
Ambapo kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, malipo ya awali kwa wateja wenye kiwango cha chini yatalipwa na kila mmoja kupata shilingi milioni 1.5, huku wateja wenye kiwango kikubwa zaidi ya hicho watalazimika kusubiri mpaka utaratibu wa kuhakiki mali na madeni ya taasisi hizo.
Emmanuel Boaz ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa DIB, amesema wateja wa benki hizo wanatakiwa kwenda na nakala zao zitakazowathibitisha ili kurahisisha maofisa watakaokuwepo kuwahudumia.
”Benki hazikuwa na wateja waliotunza mali zenye thamani kama dhahabu na vito vingine, Wengi waliweka akiba zao tu huko, Kila atakayepata taarifa aende kwenye ofisi za benki yake kwa ajili ya malipo” amesema Boaz.
Ametaja miongoni mwa nyaraka zitakazowawezesha wateja kufanikisha malipo hayo ni pamoja na kitambulisho cha Taifa, pasi ya Kusafiria, kitambulisho cha mpiga kura, leseni ya udereva au barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Pia DIB imewataka wadaiwa wote wabenki hizo kujitokeza na kulipa madeni yao au kupanga namna ya kuyalipa kabla ya April 17, amesema kutofanya hivyo ni ukiukaji wa sheria, hivyo hatua madhuti kuchukuliwa dhidi ya wakopaji hao watakao kaidi agizo hilo.
Januari, Gavana mstaafu wa Benki kuu ya Tanzania, (BOT), Profesa Beno Ndulu, alitangaza kufungia benki hizo baada ya BoT kujiridhisha kuwa hazina mtaji wa kutosha kujiendesha.