Upande wa serikali katika kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara, Mohammed Dewji ‘Mo’ umeieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado inawasaka raia wanne wa Msumbuji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka nyara mfanyabiashara huyo.

Mshtakiwa mmoja ambaye ni dereva taksi na mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb (46) tayari alishafikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi

Aidha, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon alimuelezea Hakimu Shaidi kwamba upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba wanaendelea kuwasaka washtakiwa wengine watano, ambapo baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, 2019.

Awali, Hakimu Shaidi alitoa hati ya kuwakamata washtakiwa hao ambao ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote ni raia wa Msumbiji.

Hata hivyo, katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo ya Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara ‘Mo’ kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Video: Waziri Jafo, CCM wapishana uchaguzi serikali za mitaa, Waziri aibua madudu
Madaktari wengi nimewaona mna 'Stress'- Waziri Jafo