Waziri Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewahasa wafugaji wote nchini kujenga utamaduni wa kutumia pembejeo na malighafi zenye ubora, usalama, viwango stahiki kutoka kwenye vyanzo vilivyosajiliwa kwenye uzalishaji wa mifugo.
Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake wenye tija na kuimua pato la taifa, huku akiwataka watakaotekeleza mfumo huo kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na watoa hukumu kwa wananchi.
“Utaratibu huu ni wa ushirikishwaji, sasa tunapokuwa huko kufanya ukaguzi kuhusiana na ubora na viwango tusijigeuze sisi kuwa polisi. Kwa nchi yetu mfumo huu ni rahisi na ambao umelenga kuzipatia taarifa wizara, taasisi na wadau wengine kuhusiana na ukaguzi, ubora na usalama wa mifugo pamoja na mazao yake.” Amesema Waziri Ndaki
Amesema kuwa umuhimu wa mfumo huo ni kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa kulinda afya za walaji, mifugo na mazao yake kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo litasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia pembejeo na huduma zilizosajiliwa na kutambuliwa kisheria.
Waziri Ndaki pia ametumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wataalam wa Wizara, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi na wadau waliopo kwenye vyama vya tasnia kuhakikisha wakaguzi, wazalishaji, watoa huduma kwenye mifugo wanazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha mlaji wa mifugo na mazao yake anaendelea kunufaika kiafya na kimaslahi kupitia maziwa, nyama na mayai na bidhaa nyingine.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Amosy Zephania amesema Wizara imeanzisha na kuboresha mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umejikita kwenye tasnia za kuku, maziwa, nyama, mayai, ngozi, malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo.
Bw. Zephania amesema mfumo huo umelenga kuongeza ari na hamasa ya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo kwa kutatua changamoto za ubora, usalama na viwango stahiki kwenye mifugo, mazao ya mifugo na pembejeo za mifugo.