Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Frank Mwaisumbe ameliagiza jeshi la Polisi wilayani humo kuwakamata watu wote waliohusika na tukio la kuwapiga watumishi na watendaji wa serikali wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ametoa agizo hilo katika kijiji cha Engarenaibor katika tarafa ya Engarenaibor wilayani Longido, ambapo tukio hilo limesababishwa na jamii ya wafugaji waliokuwa wakitorosha mifugo yao kuelekea nchi jirani ya Kenya.
Aidha, katika tukio hilo lililosababishwa na wafugaji hao wamefanya uharibifu katika ofisi za serikali ya kijiji hicho pamoja na kupelekea kulazwa kwa afisa mmoja wa serikali baada ya kuumizwa na wafugaji hao.
Tukio hilo limetokea wakati wa uthaminishaji wa mifugo hiyo iliyokamatwa ikiwa katika hali ya kutoroshwa kupelekwa nchi jirani ya Kenya bila kulipiwa ushuru, jumla ya mifugo iliyokamatwa ni Ng’ombe 41 na Mbuzi pamona na Kondoo 521.
Kwa upande wake mtendaji wa kijiji cha Engarenaibor, Tomas Ngobei amesema kuwa mifugo hiyo imekamatwa kwa sababu imekuwa ikipitishwa katika kijiji hicho kwenda nchi jirani ya Kenya bila kulipiwa ushuru, hivyo wamekuwa wakishirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi kuzuia utoroshwaji huo.
Utoroshwaji wa mifugo kupitia wilaya ya Longido kupelekwa nchini Kenya umekuwa ukifanyika mara kwa mara na hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na serikali ya kijiji, kata pamoja na tarafa wameungana kwa pamoja kuhakikisha suala hilo linakomeshwa.