Baadhi ya watendaji wa Tanesco wanasubiri kufutwa kazi rasmi baada ya kuapishwa rais wa serikali ya awamu ya tano, siku chache baada ya zoezi la kupiga kura na kumtangaza mshindi.

Hilo limebainika baada ya wagombea wenye nguvu zaidi, Edward Lowassa wa Chadema na Dk. John Magufuli wa CCM kuweka wazi kwa nyakati tofauti kuwa endapo watachaguliwa kuingia ikulu watawafuta kazi baadhi ya watendaji wa Tanesco kwa kile walichodai kuwa ni uzembe unaopelekea tatizo la ukosefu wa umeme nchini.

Akiongea katika mkutano wa Kampeni jijini Arusha, Dk. Magufuli aliahidi kuwa akiingia madarakani tatizo la umeme nchini litakuwa la kihistoria lakini ataanza na watendaji ikiwa ni pamoja na mawaziri.

“Najua mawaziri wapo kwenye kampeni, lakini nao wajiandae zimebaki siku 18,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa upande Edward Lowassa, akiwa katika harakati zake za kampeni mkoani Kilimanjaro, aliahidi kuwa atahakikisha anamaliza tatizo la umeme chini kwa kuwa hiyo ni nishati muhimu inayochangia kwa asilimia kubwa katika uchumi wan chi.

Pia, aliwataka baadhi ya watendaji wa Shirika hilo la umeme nchini kujiandaa kuondoka katika nafasi zao kwa kushindwa kulitatua tatizo la umeme na kukata umeme pasipokuwa na sababu za msingi.

“Nasikitika hali ya umeme nchini, kila siku wanakata umeme na maelezo hayatoshelezi. Na mara nyingine hawatoi maelezo, wanatuach tu. Kila mtu anapata adha na tabu bila sababu. Kila siku umeme unakatika mara tatu mara nne, nauliza serikali iko wapi? Kwanini hawa wanaosema uongo hawawajibishwi?” Lowassa alihoji.

“Serikali nitakayoiongoza mimi, mtu akinifanyia mchezo wa namna hiyo namfukuza kazi mara moja, palepale. Uchumi unasimama kwa kukosekana umeme wa uhakika, uwezo upo lakini viongozi wetu wameshindwa kulitatua. Ninawaambia Tanesco wajipange, baadhi ya watendaji watafute kazi nyingine,” alisema Lowassa.

Kwa kipindi cha takribani siku 5, nchi imekumbwa na tatizo la mgao wa umeme ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa Tanesco utangaze kuwa tatizo hilo litakuwa historia kwa kuwa tayari wameshaunga umeme huo katika mfumo wa gesi.

Marbury Amchana Hadharani Michael Jordan
Kumbe Liverpool Hawakua Na Lengo Na Klopp!!