Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wateule ambao anawakisimia madaraka kuheshimu katiba, kujua mipaka na kuweka siri za serikali.
Rais Samia ameyasema hayo Octoba 03, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha Mawaziri watatu aliowateua ambao ni Dkt. Stergomena Tax, Innocent Bashungwa, na Angela Kairuki ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge na Waziri.
Rais Samia amesema, “Ni lazima Kujua Mipaka ya kimamlaka, kujua nchi hii ina mamlaka na mamlaka uliyowekewa ina ukomo wake, lazima unapotaka kuvuka upate ruhusa ya mamlaka ya juu, sasa mjue mipaka yenu wakati unapofanya kazi, kwenda juu lakini pia kushuka chini,”
Pamoja na suala hilo Rais Samia pia amewataka kutetea katiba ambapo alisema, “Katika viapo vyetu hapa tunaapa kuitetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ninaamini kuwa mnakubali kutumika kwa pande zote mbili za Muungano huu kwa jinsi katiba ilivyogawa majukumu,”
Aidha Rais Samia amewataka wateule hao kutunza siri za Baraza la Mawaziri, au Baraza la Mapinduzi, na kuheshimu yote yanayoamuliwa na Serikali na kuyatenda kama ni Masuala binafsi na sio maelekezo.
“Linaloamuliwa na serikali wewe kama Waziri ni lako,na unatakiwa ulibebe ukalifanyie kwazi kwa misingi uliyoelekezwa, huwezi kwenda kusema nimeelekezwa hivi, mimi sikutaka hivi lakini nimekuja kufanyia maelekezo, huwezi kujitoa.”
Awali akiongea kabla ya Rais Samia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amewapongeza Mawaziri hao waliokasimiwa madaraka katika wizara hizo tatu na kuwaahidi ushirikiano kutoka ofisi ya Bunge.