Umoja wa Mataifa UN, umesema zaidi ya watoto 11,000 wameshauawa ama kukatwa viungo vyao kutokana na matukio ya uwepo wa maradhi ya aina mbalimbali au kujeruhiwa wakati wa vita ambavyo vinatimiza mwaka wake wa nane nchini Yemen, Taifa ambalo ni masikini katika ukanda wa eneo la Ghuba ya Arabuni.
Kwa mujibu wa ripoti, iliyotolewa hii leo Jumatatu ya Desemba 12, 2022 na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), imeeleza kuwa huenda idadi kamili ya watoto waliouawa na kupoteza viungo vyao inapindukia takwimu rasmi zilizochapishwa, huku maelfu ya wengine wakiwa kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na maradhi yanayoepukika ama njaa.
Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell amesema kwasasa watoto zaidi ya milioni mbili nchini Yemen wana utapiamlo wa kiwango kibaya, ambapo robo yao ni wale walio chini ya umri wa miaka mitano na kuongeza kuwa, “wengi wao wanaweza kupatwa na kipindupindu, churuwa na maradhi mengine yenye chanjo.”
Vita nchini Yemen, vilizuka mwaka 2014 na kushuhudia kundi la waasi wa Kihouthi likifanikiwa haraka kutwaa udhibiti wa mji mkuu, Sana’a, ambapo mwaka mmoja baadaye muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliivamia nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na waasi hao wanaoshukiwa kuungwa mkono na hasimu mkubwa wa Saudia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha, UNICEF imethibitisha vifo 3,774 kwa kipindi cha Machi 2015 na Septemba 2022 huku makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yakidumu hadi Oktoba 2, lakini pande hasimu zilishindwa kuongeza muda zaidi baada ya hapo na tangu kumalizika kwa makubaliano hayo, watoto 62 wameshauawa ama kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa UNICEF, wavulana 3,904 wamejiunga na makundi ya wapiganaji na wasichana wengi wamepewa majukumu ya kivita kama vile kuwa walinzi kwenye vizuizi vya barabarani na sasa Shirika hilo linaomba jumla ya dola milioni 484.4 za kukabiliana na hali mbaya ya kibinaadamu inayowaandama watoto wa Yemen.