Jumla ya watoto laki 550,388 wanatarajia kupata chanjo ya Polio, Surua na Rubella katika Mkoa wa Dodoma ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo dhidi yao na kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kupitia kampeni ya chanjo kitaifa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameyasema hayo jijini Dodoma jana, na kubaisha kuwa zoezi hilo linatarajia kufanyika kwa siku tano kuanzia Oktoba 17 hadi 21, 2019 katika vituo vyote 339 vitakavyotoa huduma ya chanjo.
Amesema chanjo ya Surua na Rubella itatolewa kwa watoto walio na umri wa miezi tisa mpaka miaka minne na miezi 11 ambao jumla yao ni laki 368,352 huku chanjo ya Polio ikitolewa kwa watoto walio na umri wa mwaka mmoja na miezi sita mpaka miaka mitatu na miezi sita ambao ni laki 182,036.
“Chanjo hizi zinatolewa kwa njia ya Sindano na hazina madhara kwa mtoto bali zitamlinda dhidi ya magonjwa ya Surua, Rubella na Polio na hivyo kuepusha ulemavu na vifo vinavyoweza kutokea kutokana na magonjwa hayo,” amesema Mahenge.
Amefafanua kuwa Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma zitashiriki zoezi hilo ambazo ni Kongwa watoto wa miezi 9-59 wapatao 58,811 kwa chanjo ya Surua na Rubella na watoto 27,669 wa miezi 18-42 kwa chanjo ya Polio na Dodoma Jiji watoto wa miezi 9-59 wa chanjo ya Surua na Rubella 56,163 na watoto 24,836 wa miezi 18-42 wa chanjo ya Polio.
Wilaya nyingine ni Chamwino kwa watoto 63,034 wa miezi 9-59 chanjo ya Surua na Rubella huku watoto 30,104 wa miezi 18-42 kwa chanjo ya Polio, Bahi kwa watoto 44,035 wenye miezi 9-59 wa Surua na Rubella, watoto 19,667 wa miezi 18-42 chanjo ya Polio na Chemba watoto 44,049 wa miezi 9-59 kwa Surua na Rubella huku watoto 20,534 wa chanjo ya Polio.
“Mpwapwa chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto wa miezi 9-59 ni 55,603 na watoto wa miezi 18-42 wa chanjo ya Polio ni 26,538 wakati Kondoa Vijijini ni watoto 38,067 wa miezi 9-59 wa Surua na Rubella huku watoto 17,636 wa miezi 18-42 chanjo ya Polio na Kondoa mji watoto 8,590 wa miezi 9-59 wa chanjo ya Surua na Rubella na watoto wa miezi 18-42 wapatao 5,052 watapata chanjo ya Polio,” ameongeza Mahenge.
Aidha Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge amesisitiza wana Dodoma kutumia fursa hiyo kwa kuwapeleka watoto wenye umri huo kupata chanjo na kudai kuwa tayari maandalizi katika Wilaya zote yamekamilika na uzinduzi wa zoezi hilo unatarajia kufanyika Wilayani Bahi ukiwa na kauli mbiu ya “Chanjo ni kinga, kwa pamoja tuwakinge”