Jumla ya Watoto 80, waliokuwa sehemu ya mamia ya waandamanaji waliokamatwa na kushikiliwa katika gereza moja la jangwani nchini Chad baada ya maandamano yaliyokumbwa na vurugu na vifo mwezi wa Oktoba, wameachiliwa huru.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Chad, Wade Djibrine, amesema ombi la kutaka watoto hao waachiliwe huru liliwasilishwa kwa mujibu wa taratibu na Jaji akalikubali, licha ya kuwa mashtaka dhidi ya watoto hao bado yanaendelea.
Katika maandamano hayo, mamia ya watu walikamatwa na kushikiliwa na maafisa wa usalama, kufuatia maandamano ya vurugu dhidi ya utawala wa kijeshi wa Chad Oktoba, 2022 na tayari watu 262 wamehukumiwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela.
Hata hivyo, maandamano hayo ambayo hayakuruhusiwa na serikali yalifanyika Oktoba 20, 2022, yakiwa na lengo la kulikumbusha jeshi tarehe ambayo awali liliahidi kuachia madaraka na kuruhusu utawala wa kidemokrasia.