Serikali nchini, imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizi, huku mwaka 2023/2024 ikijipanga kuongeza vituo 100, ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni 2024 vitavyosaidia kuongeza huduma hizo nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo hii leo Juni 28, 2023 jijini Dodoma, huku akiongeza kuwa pia imeendelea kuongeza vifaa na vifaa tiba ikiwemo CT-SCAN kutoka 3 mpaka kufikia zaidi ya 50.
Amesema, “MRI zilikuwa 2 lakini mpaka sasa zipo zaidi ya 19, hivyo kumtoa kuwaondoa hofu Wabunge kuwa hata vifaa vya huduma hizo vitaenda kuwekwa kwenye vituo vyote 100 vitavyojengwa nchini.
Hata hivyo, Dkt. Mollel amesema, katika kukabiliana na changamoto ya gharama za matibabu kwa wazee, Wizara inaendelea kuhamasisha Wabunge na viongozi wengine pamoja na wananchi kuunga mkono Bima ya afya kwa wote, ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma bora bila gharama kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka hospitali ya Taifa.