Timu ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’ leo asubuhi imeichapa timu ya jeshi ya Green Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL) bao 1-0, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Bao pekee la vijana hao lilifungwa na Alphonce Ukani aliyewazidi ujanja mabeki wa Warriors na kupiga shuti lililomshinda kipa wa timu hiyo.

Kikosi hicho ambacho kimekuwa kikifanya vizuri kwenye kila mchezo wanaocheza, kimeifunga Warriors iliyokuwa na mchanganyiko wa baadhi ya wachezaji waliowahi kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiwemo Haruna Adolph.

Makocha wa Azam FC Academy, Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche, wameutumia mchezo huo katika kuwapima wachezaji wa kikosi hicho pamoja na kuwafanyia tathimini ya viwango vyao.

Azam FC Academy imepata ushindi huo katika mchezo wao wa kwanza kwa mwaka huu, ambapo iliufunga mwaka jana kwa kuichapa timu ya Ugimbi inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) mabao 8-0, mchezo uliofanyika Desemba 30.

Rekodi kubwa waliyomaliza nayo mwaka jana ni ile ya kuwafunga vijana wenzao wa Kingunge Superstar mabao 32-0 huku mwanzoni mwa mwaka jana ikiipiga timu ya Chuo cha Biashara cha CBE mabao 31-0.

Mohamed Elneny Katika Muonekano Wa Kiarsenal
Mayanja Akosoa Mipango Ya Kocha Dylan Kerr