Faisary Ahmed – Bukoba.

Watoto wawili wa familia moja, wamekutwa wamefariki baada ya kufunikwa na jiwe wakati wakichimba mchanga eneo la Maharahara, lililopo katika Kijiji cha Magata kata ya Magata Karutanga, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Alhaj Yakoub Mahamud amewataja watoto hao kuwa ni Samson Eliudi (13) na Emmanuel Eliud (10), ambao wote walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Magata na walikuwa wakichimba mchanga walipotoka shuleni baada ya baba yao mzazi kutelekeza familia na kubaki na mama yao.

Eneo ambalo watoto wawili walifariki kwa kufunikwa na jiwe wakati wanachimba mchanga.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga amepiga marufuku shughuli za uchimbaji mchanga eneo hilo na kuwasihi wazazi kutokimbia familia zao kwani matukio ya namna hiyo husababishwa na vitendo hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga (kushoto), akianglia eneo ambalo watoto hao walifukiwa na mawe.

Amesema, “kuanzia muda huu haya maeneo yamefungwa rasmi ni wajibu wa serikali ya kijiji kuendelea kupitia maeneo haya ili tusione awe mtu mzima au mtoto mdogo kuendelea kuchimba mchanga na tunapoyaona matukio kama haya watoto wanatangatanga tuzikusanye hizo taarifa na tuzifanyie kazi.”

Kwa upande wao, Wananchi licha ya kusikitishwa na tukio hilo, wameiomba serikali kupitia ustawi wa jamii kubaini wazazi wanaotelekeza watoto kuchukuliwa hatua na kuwasaidia kutojihusisha na kazi hatarishi huku wanafamilia wakiruhusiwa kuendelea na utaratibu wa mazishi.

Simba SC kutangaza usajili mpya Jumatatu
Liverpool kujitutumua kwa Kylian Mbappe