Watoto watano wamefariki kutokana na mafuriko wilayani Korogwe, Mkoani Tanga na kufanya idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko kufikia 12.
Vifo hivyo vimetokea katika kata ya Foroforo, baada ya nyumba iliyokuwa na watu nane wa familia moja kuanguka na watoto watano kati yao kusombwa na maji ambapo miili yao yote mitano imepatikana.
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kwa takribani wiki mbili sasa katika maeneo mbali mbali, kaya zaidi ya 300 zimekosa makazi mkoani humo.
Aidha daraja la Mto Mandera lililopo kata ya Segera mpakani mwa wilaya ya Handeni na Korogwe limekata mawasiliano jana, ya barabara kati ya mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Arusha, Pwani na Manyara na kusababisha magari zaidi ya 200 kukwama kwa zaidi ya saa 36 huku abiria zaidi ya 800 wakilala nje.
Hata hivyo, watu 120 ambao makazi yao yamezingirwa na maji wamehifadhiwa katika kambi maalumu, kijijini hapo na kutakiwa kutorudi katika makazi yao hadi tamko la Serikali litakapotolewa.