Kufuatia kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii juu ya taarifa ya watoto wenye umri mdogo kufunga ndoa, mtoto wa kiume anayesoma darasa la nne na wa kike darasa la pili wamezungumza kuhusu ndoa hiyo iliyopewa vichwa mbalimbali vya habari.
Watoto hao walipohojiwa na EATV kwa nyakati tofauti wamesema kuwa haikuwa ndoa ya ukweli kama ilivyodhaniwa bali ilikuwa ni sherehe ya kitoto.
Naye kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, amekiri kuwa tukio hilo kweli ilikuwa ni shughuli za kitoto, lakini bado wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu zaidi kujua undani wake.
“Kwa harakaharaka tunaweza tukasema kuwamba zilikuwa ni shughuli za watoto zilizokuwa zinafanyika hapo mtaani, tumefuatilia na bado tunafuatilia ili kuona wahusika halisi wa tukio hilo, kuna mambo ya msingi tunataka kuona ikiwemo suala la chakula,” amesema Kamanda Mponjoli.
Kamanda ameongezea kuwa bado wanaendelea kufuatilia tukio hilo lililofanyika Mei 11, 2020 ili kujua kama kweli lilikuwa ni suala la watoto au kulikuwa na umakini ndani yake.