- Johansen Buberwa, Bukoba – Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa, amesema amepokea kwa masikitiko vifo vya Watoto watano ambao wamefariki katikia Kijiji cha Nyakanazi kilichopo Wilayani Biharamuro, wakisadikika kuwa wamekula chakula chenye sumu, huku akitoa angalizo kwa Wananchi kuwa makini na mboga wanazochuma kuhakikisha zipo salama.
Akizungumza na Vyombo vya Habari, Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kufika Serikali imeanza kulifanyia uchunguzi tukio hilo na timu wataalamu mabingwa wengine kutoka nje ya Mkoa watafika kusaidia uchunguzi juu ya tukio hilo.
Amesema, “Wananchi wachukue tahadhari hasa kwa Mboga za majani wanazochuma kuwa na uhakika nazo kuwa ni salama wasichume mboga katika mashamba yaliyopuliziwa dawa au kuwekewa Mbolea ambazo zinaweza kuwazuru binadamu.”
Aidha, Hajat Mwasa amewaomba Wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuwa na subira kwenye kipindi kigumu na kusema Serikali itashiriki mazishi hayo kwa hali na mali na tayari wameelekeza makaburi yaanze kuchimbwa na watatoa ubani kwa familia za marehemu.