Serikali nchini Chad imefunga migodi bubu ya dhahabu eneo la kaskazini mwa nchi hiyo baada ya
kutokea vifo vya wachimbaji 100 na wengine 40 kujeruhiwa kufuatia kuibuka kwa mabishano
yaliyosababisha vurugu na kupelekea mapigano baina ya pande mbili.
Waziri wa Ulinzi nchini Chad Daoud Yaya Brahim amesema vurugu hizo zimetokea usiku wa Mei
23 na Mei 24, 2022 katika eneo lisilo rasmi la migodi ya dhahabu lililopo wilaya ya Kouri Bougoudi
jirani na mpaka wa nchi hiyo na Libya
“Taarifa za vyombo vyetu vya usalama zinasema kilichotokea ni kama mzozo wa kawaida kati ya
watu wawili na baadaye hali ikazidi kuchafuka na kupelekea mzozo mkubwa uliosababisha
maafa,” amefafanua Waziri huyo wa ulinzi.
Chad imesema mara baada ya kupata taarifa za machafuko katika eneo hilo Mei 25, 2022 ilituma
ujumbe ili kurejesha hali ya amani na kupata ukweli halisi ambapo iligundulika idadi hiyo ya vifo
na majeruhi.
“Uchunguzi uligundua idadi ya vifo vya watu 100 na hao majeruhi na tayari tumewaondoa watu
wote kwani hii si mara ya kwanza kuwepo vurugu za wachimba dhahabu katika kanda na
uchimbaji utasimama hadi ilani nyingine itakapotolewa,” amesisitiza Waziri Brahim.
Awali Waziri wa Mawasiliano nchini Chad Abderaman Koulamallah amesema Milima ya Tibesti
iliyoko katikati mwa jangwa la Sahara takriban kilomita 1,000 kutoka mji mkuu wa nchi ya Chad
Djamena ipo chini ya uangalizi baada ya kupata hasara za maisha ya binadamu na majeruhi.
Hata hivyo kumekuwepo na mkanganyiko wa taarifa za idadi ya vifo na majeruhi katika eneo hilo
kwani baadhi ya vyombo vya habari na mashuhuda wa tukio wanasema Serikali inaficha ukweli
kwani idadi iliyotangazwa ni ndogo ikilinganishwa na uhalisia.
Kugunduliwa kwa dhahabu wilayani Kouri Bougoudi kumezua msongamano wa wachimba migodi
kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Mauritania na Libya ambazo raia wake waanadaiwa kuwa ni
sehemu ya mzozo uliosababisha mapigano.