Watu 14 wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya watu waliojihami kwa silaha kufyatua risasi katikati ya Mji wa Soweto, Johannesburg, nchini Afrika Kusini.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa watu hao wenye silaha walishuka kwenye gari dogo la kukodi na kufyatua risasi wakiwalenga watu wote waliokuwa kwenye ‘bar’ moja iliyo katikati ya mji, usiku wa kuamkia leo.
Mapema leo asubuhi, polisi walionekana katika eneo hilo wakiondoa miili ya waliouawa na kufanya uchunguzi wa awali.
Kamishna wa Polisi wa Jimbo la Gauteng, Lt. Gen. Elias Mawela alisema uchunguzi wa awali unaonesha wafyatua risasi walikuwa wengi.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa hawa watu walikuwa wanapata raha zao hapa kwenye eneo la starehe ambalo limepewa leseni halali ya kufanya biashara usiku kucha. Ghafla walisikia milio ya risasi, na ndipo walijaribu kukimbia. Washambuliaji waliwalenga watu hawa, na hadi sasa hatujafahamu sababu,” alisema Mawela.
Polisi wameeleza kuwa majeruhi watatu waliokimbizwa katika Hospitali ya Chris Hani Baragwanath wako katika hali mbaya na wanaendelea kupatiwa matibabu.