Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewahukumu adhabu ya kifo watuhumiwa 51 waliokabiliwa na kesi ya mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa waliouawa mwaka 2017.
Idadi kubwa ya watu walikuwa wakifuatilia kesi hiyo mahakamani tangu ilipoanza kusikilizwa zaidi ya miaka minne iliyopita kuhusu mauaji hayo yaliyotikisa jamii ya wanadiplomasia na wafadhili ingawa sababu hasa ya tukio hilo bado haiko wazi.
Hukumu kubwa kama hiyo hutolewa katika kesi za mauaji nchini DRC lakini hubadilika na kuwa kifungo cha maisha tangu taifa hilo lilipotangaza kusitisha hukumu ya kifo mwaka 2003.
Michael Sharp, raia wa Marekani na Zaida Catalani raia wa Sweden na Chile walipotea wakati wakichunguza machafuko katika mkoa wa Kasai chini ya Umoja wa Mataifa.
Waendesha mashtaka katika mahakama ya kijeshi ya Kananga walipendekeza hukumu ya kifo dhidi ya washtakiwa 51 kati ya washtakiwa 54.
Mashtaka yaliyowakabili watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na ugaidi, mauaji, kushiriki katika vuguvugu la uasi na kutenda uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.