Takriban watu 53 wamefariki huku watu 58 wakiwa wamejeruhiwa , wengine wakiwa na majereha mabaya baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupata ajali mbaya kusini mwa Mexico.
Takriban watu 100, wanaodaiwa kuwa wahamiaji kutoka Marekani ya kati walikuwa ndani ya lori hilo wakati lilipopindukia na kugonga daraja katika jimbo la Chiapas.
Mkuu wa kitengo cha utetezi wa raia wa Chiapas Luis Manuel Garcia, amesema ajali hiyo ni mojawapo ya ajali mbaya zaidi kutokea nchini Mexico.
 Amesema kwamba waathiriwa walikuwa pamoja na wanaume, wanawake, na watoto ambapo Uraia wao haujathibitishwa , lakini maafisa wa eneo hilo wanasema kwamba wengi wa waliokuwa ndani ya lori hilo ni wahamiaji kutoka mataifa ya Honduras na Guatemala.
Chanzo cha ajali kinaelezwa kuwa Lori lilikuwa kwenye mwendo wa kasi kabla ya kupoteza mwelekeo katika kona na kugonga daraja la raia katika barabara kuu inayoelekea katika mji mkuu wa jimbo la Chiapas , Tuxtla Gutierrez.
Mamia ya maelfu ya wahamiaji wanaotoroka umasikini na ghasia Marekani ya kati hujaribu kuvuka kupitia Mexico kila mwaka kwa lengo la kuwasili Marekani.