Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kupitia msemaji wa jeshi hilo SACP David Misime ametoa tathmini ya Operasheni ya nchi nzima kuanzia Mei hadi Julai 2021, huku akielezea mafanikia ya oparesheni hiyo kuwa imewakamata jumla ya watuhumiwa 5,429.

Kamanda Misime amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya mauaji, tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha, makosa ya kubaka na mengineyo.

Akielezea ufafanuzi wa makosa hayo Kamanda Misime amesema waliokamatwa kujihusisha na mauaji ni 275, kati yao waliokamatwa kutokana na mauji ya wivu wa kimapenzi ni 21, imani za kishirikina ni 22 na 231 kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa pamoja na kujitafutia kipato kwa njia za kiuhalifu.

Hali kadhalika watuhumiwa 63 walikamatwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha, 141 wakikamatwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu. Huku 1,265 walikamatwa kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba.

Waliokamatwa kwa makosa ya kubaka ni 508, wakati 125 wakikamatwa kwa tuhuma za kulawiti. Kufuatia operesheni hiyo, watu 2,300 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha kilo 540 kilikamatwa, Cocain gramu 104, bhangi kilo 3304.321 zilikamatwa. Mashamba ya bhangi hekari 11.75 ziliharibiwa. Mirungi kilo 2233.394 zilikamatwa,” amesema Kamanda Misime.

Watu 398 walikamatwa kwa tuhuma za kutengeneza pombe haramu ya gongo na kuuza, kiasi kilichokamatwa ni lita 13612.175 na mitambo ya kutengeneza pombe hiyo iliyokamatwa ni 94, huku waganga wa ramri chonganishi waliokamatwa ni 15.

Aidha katika watuhumiwa wote 5,429 waliokamatwa kulingana na ushahidi ulivyowagusa, wameshafikishwa mahakamani.

Watano mbaroni kwa utapeli wa ardhi
COSOTA watakiwa kutoa elimu ngazi za mikoa