Polisi wanaosimamia sheria ya kiislam (Sharia) katika jimbo la Kano nchini Nigeria wamewashikilia watu 80 kwa tuhuma za kula mchana hadharani, wakati wa mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Polisi hao ambao wanafahamika kama Hisbah wameeleza kuwa watu hao walishikiliwa katika maeneo mbalimbali kwenye jiji la Kano ndani ya kipindi cha siku chache zilizopita.
Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo yanafuata sheria ya kidini (Sharia) tangu mwaka 2000, lakini wanazingatia pia sheria za nchi.
Msemaji wa Polisi wa Hisbah katika jimbo hilo, Adamu Yahaya ameiambia BBC kuwa watu hao waliokamatwa ni waumini wa dini ya Kiislam na kwamba maafisa wa jeshi hilo hawawakamati watu ambao sio waumini wa dini hiyo kwakuwa sheria za kiislam haziwahusu.
Alisema kuwa baadhi ya watu waliokamatwa waliwaambia maafisa wa polisi kuwa walikuwa wanakula kwa sababu wao binafsi hawakuuona mwezi ukiandama, na wengine walitoa sababu za ugonjwa ambazo zilionekana kuwa hazina mashiko.
Hata hivyo, Yahaya alisema kuwa watu hao wote 80 waliachiwa huru kwa sababu walibainika kuwa walifanya kosa hilo kwa mara ya kwanza.
Hisbah wameeleza kuwa wataendelea na msako wao katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na watawakamata waislamu wote ambao hawafuati masharti ya kufunga katika kipindi hiki bila kuwa na sababu za msingi.