Watu wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa ulinzi wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) huku mwanafunzi wa darasa la tatu anayesoma Shule ya Msingi Lemingori iliyopo Oldonyosambu wilayani Arumeru, Isaya Thomas (13) akiwa miongoni mwa majeruhi wa shambulio lililofanywa na askari hao.
Kutokana na tukio hilo, Polisi inawashikilia askari sita wa Suma JKT kwa uchunguzi dhidi ya tukio hilo lililotokea Kijiji cha Kandaskirieti Kata ya Oldonyosambu Tarafa ya Mukulati huku miili ya watu wanne waliokufa kutokana na shambulio hilo, ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo akizungumzia tukio hilo, amesema juzi saa 11 jioni katika Kijiji cha Kandaskirieti, watu wanne walikufa baada ya kupigwa risasi na askari wa Suma JKT.
Amesema taarifa za awali zimebaini kuwa askari hao wa Suma JKT ambao ni walinzi wa shamba la miti la Serikali la Meru Usa Plant, walianza kufanya operesheni ya kuondoa mifugo, ambako walikamata ng’ombe 45, mbuzi na kondoo 65 kisha kuwapeleka zizi la Serikali lililopo Kituo cha Polisi Oldonyosambu.
Aidha, amesema saa 11 jioni waliendelea tena na operesheni hiyo na kukamata ng’ombe wengine 80, mbuzi na kondoo wakiwa 70 na kuwapeleka kwenye zizi la serikali na wakati wanarudi, ndipo walipokutana na kundi la wananchi wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kushambuliwa, hivyo askari hao walirusha risasi hewani ili kuwatawanya.
Kamanda Mkumbo amewataja waliokufa kuwa ni Mbayani Melau (27), Julius Kilusu (45), Lalashe Meibuko (25) na Seuri Melita (32) ambao miili yao imehifadhiwa Mount Meru.
Pia amewataja majeruhi waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni William Ngirangwa (29), Mathayo Masharubu (34), Julius Lazaro (32), Evelyn Melio (28) na Isaya Thomas (13), ambao wamelazwa Mount Meru wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao huku hali zao zikiwa si nzuri.

Usain Bolt Kupokonywa Medali Ya Dhahabu
Copa del Rey: Real Madrid Yatupwa Nje