Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu wanaotuhumiwa kuratibu maandamano yaliyofanywa leo na mamia ya watu nje ya Ubalozi wa Afrika Kusini wakishinikiza ndege ya ‘Air Tanzania’ inayoshikiliwa nchini humo kuachiwa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa maandamano yoyote yasiyo na kibali hayakubaliki. Alisema waratibu hao wangeweza kufikisha mawazo na mitazamo yao kwa njia ya barua.

“Kwanza sisi Jeshi la Polisi haturuhusu maandamano, na pia haturuhusu mtu kufanya anavyojisikia yeye, baada ya kupata taarifa nilimwagiza RPC Ilala ili kuchukua hatua za kuzuia maandamano. Pili, kuwakamata waratibu wa maandamano hayo,” amesema Kamanda Mambosasa.

Ameeleza kuwa Serikali imetuma wawakilishi nchini Afrika Kusini kushughulikia suala la kukamatwa kwa ndege hiyo.

“Hili ambalo hawa wamelifanya halikubaliki. Tuheshimu sheria hata pale tunapoona kuwa jambo linalofanyika halipendezi lakini kuheshimu sheria ni jambo la maana sana,” aliongeza Kamanda Mambosasa.

Jana, Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas aliwataka Watanzania kuwa watulivu akiwahakikishia kuwa ndege ile itarejea.

Dkt. Abbas alisema kuwa Tanzania haitarudi nyuma au kukata tamaa kwa namna yoyote na kuwahakikishia wananchi kuwa ndege itarudi.

Ndege hiyo imeshikiliwa baada ya mkulima mmoja wa Afrika Kusini kudai fidia ya kutaifishwa shamba lake nchini katika miaka ya 1980.

Majaliwa akutana na waziri mkuu wa Mauritius
Mwinyi Zahera awatahadharisha wachezaji Yanga