Jeshi la polisi mkoani Kigoma limewatia mbaroni watu watano wanotuhumiwa kujihusisha na matukio ya ubakaji wanawake nyakati za usiku huku wakiwa wamejipaka mafuta ya mawese na oil chafu, maarufu kama tereza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema kuwa tayari wamewakamata watu watano ambao wametajwa kuhusika na vitendo hivyo na kwamba tayari uchunguzi unaendelea na kwa sasa hayuko tayari kutoa taarifa za kina kuhusiana na jambo hilo.

Kamanda Ottieno amesema uchunguzi wao unapitia hatua ngumu kutokana na ushirikiano hafifu unaotolewa na baadhi ya wananchi, kwa kuwa wengi wamekuwa wakiona aibu kueleza kama waliingiliwa na wahalifu hao kwenye nyumba zao.

Ameongeza kuwa tayari wameimarisha ulinzi katika maeneo hayo, ikiwemo doria za usiku na kuwatoa hofu wananchi wa manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa tayari vitendo hivyo vimedhibitiwa na kuwataka kutoa taarifa za fununu za watu wanaohusika na vitendo hivyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga alisema watu wanaovamia nyumba za wanawake usiku kwa nia ya kufanya vitendo vya ubakaji, wakiwa wamejipaka mafuta ni wahalifu kama wahalifu wengine na Serikali itachukua hatua kali kubiliana nao.

 

 

Waliohamishwa makazi Bukoba waruhusiwa kurudi
Mtuhumiwa wa tukio la utekaji wa 'Mo Dewji' afikishwa Mahakamani