Watuhumiwa wa wizi wa Luninga 15 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi 11 milioni na Kompyuta 3 za Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe akiwemo Mkuu wa Idara ya Manunuzi, Aloyce Kavumika wamesema siku ya tukio walikuwa nje ya Mkoa na kwamba walipigiwa simu kuwa Kontena lipo wazi na vitu vimeibwa.

Watuhumiwa hao, walitoa utetezi huo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka kuagiza kusimamishwa kazi kwa Watumishi wa Idara za Manunuzi, Tehama na Katibu wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo huku Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Winfred Kyambile akisema hatua alizochukua baada ya wizi huo ni kuwaita wote na kuwahoji lakini hakuripoti Polisi.

Wizi huo, uliripotiwa kuwa Kontena lililokuwa na vifaa hivyo lilifunguliwa siku ambazo si za kazi na baada ya kubainika tatizo hilo Mkuu wa Idara ya Manunuzi wa Hospitali hiyo na watunza funguo walikubaliana kuzilipa na kwenda kumuomba Mfanyabiashara wa Vifaa vya umeme mjini Njombe, ili awape Luninga 15 nyingine ambazo wangezilipa baadaye.

Mkuu huyo wa Mkoa, Antony Mtaka alitoa agizo hilo akiwa katika Hospitali hiyo kufuatia uwepo kwa taarifa hizo za wizi tangu Julai 2023 bila kuripotiwa kwenye chombo chochote cha ulinzi na usalama, huku idara ya Tehama ikishindwa kutambua tukio hilo kutokana na Kamera za eneo hilo kutofanya kazi.

Hata hivyo, Katibu Tawala na Rasilimali watu wa Njombe, Lewis Mnyambwa amekiri kupokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kuahidi kwenda kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi hao kwa mujibu wa taratibu na sheria za kazi huku akielekezwa kufungwa kwa mifumo ya Kamera katika Hospitali hiyo, kupitia Maofisa Tehema wengine, ili kuongeza ulinzi.

Kocha Wydad Casablanca aomba radhi
Kenya: Kamati yataka tahmini uchaguzi wa 2022