Bunge la Uganda limepitisha kodi kwa watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii.
Muswada huo uliopitishwa na Bunge umelenga kuwa sheria itakayochaji kiwango cha kodi cha Ush. 200 kila siku kwa watu wanaotumia mitandao kutuma jumbe kupitia Facebook, WhatsaApp, Viber, Instagram, Twitter na mingine.
Rais Yoweri Museveni hivi karibuni aliunga mkono hatua za mabadiliko hayo akieleza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikihamasisha umbea, kwa mujibu wa BBC.
Sheria hiyo inatarajiwa kuanza kufanya kazi kesho (Julai 1), ingawa bado kuna wasiwasi wa namna itakavyotumika.
Mbali na kuleta mabadiliko kwenye utumiaji wa mitandao ya kijamii, sheria hiyo pia inaweka kodi ya asilimia 1 kwenye huduma za kutuma fedha kwa njia ya simu, hatua iliyokosolewa na makundi ya wanaharakati kwa madai kuwa itaongeza gharama za maisha kwa wananchi hasa maskini.
Aidha, Waziri wa Fedha, David Bahati ameliambia Bunge kuwa kodi zilizowekwa kwenye sheria hiyo zimelenga katika kuisaidia nchi hiyo kulipa deni la Taifa.
Bado suala la kuweka kodi kwa kila siku kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kunaonekana kama kitendawili kinachosubiri majibu wakati wa utekelezaji wake.
Hatua hii imekuja wakati ambapo Serikali ya Uganda imeendelea kufanya jitihada za kuhakikisha namba zote za simu zinasajiliwa ipasavyo.