Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewapandisha madaraja watumishi 262,800 hadi kufikia Septemba 2022.

Mhagama ametoa kauli hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa, Wilaya na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma cha kuwakumbusha watumishi wajibu wao kikazi.

Amesema, “Rais Samia hadi kufikia Septemba, 2022 ameshawapandisha madaraja watumishi 262,800 ambao kwa miaka zaidi ya mitano walikuwa hawajapanda na kila mwezi Serikali inatumia shilingi bilioni 58.3 kulipia mishahara iliyopandishwa.”

Waziri Mhagama ameongeza kuwa, “Tarehe 22 Aprili, 2021 Rais Samia alilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza na kuweka vision yake, anatambua rasilimali watu ndiyo inasimamia rasilmali fedha na ndiyo maana Serikali inagharamia sana uendelezaji wa rasilmali watu nchini.”

Aidha, amefafanua kuwa, “Katika bajeti ya mwaka 2022/2023, watumishi 120,210 walitengewa fedha ili wapandishwe madaraja, tulikuwa na watumishi 67,000 wa mwaka 2015, 2016 na 2017 waliokuwa na barua za kupanda madaraja lakini zilifutwa na hawakupandishwa.”

“Rais ameagiza hawa wote wapandishwe madaraja na kabla sijaja ziara hii, nilicheki taarifa za mfumo wa utumishi na hali ya mshahara na kukuta wote wamepandishwa madaraja ila wanatofautiana kwenye ngazi na miaka ya utumishi,” alisema Waziri huyo.

Chipeta awasilisha hati za utambulisho kwa Mfalme
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 20, 2022