Watendaji wa serikali wametakiwa kutokuwa vikwazo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali, ikiwemo miradi ya maji na barabara.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho akiwa na kamati ya siasa ya mkoa kwenye ziara ya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa na serikali katika wilaya ya Songea mkoani humo.

”Wizara yetu ya Maji imefikia mahala imebweteka sana, serikali inaweza kutenga fedha lakini mpaka mkandarasi azipate fedha hizo inachukua muda, inabidi tukutane na RAS ili atuambie wao kama mkoa tatizo lipo wapi kwasababu jukumu lao ni kuhimiza wizara ilete fedha hizo,” amesema Mwisho.

Aidha, Mwenyekiti huyo amewataka watendaji wa serikali katika ngazi zote wahakikishe wanasaidia chama hicho kutimizia ahadi zake kwa wananchi ili wasione kama wanadanganywa na serikali yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea, Polilety Mgema amesema mradi huo wa maji kuwa ni mradi ambao ulianza kutekelezwa muda mrefu na wakandarasi waliondoka eneo la mradi kwa kukosa malipo hata kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Mradi huo upo katika kijiji cha Maweso halmashauri ya Madaba Wilayani Songea mkoani Ruvuma.

 

Ripoti ya CAG yaibua madudu TPB
Wasusi wa nywele watoa ya moyoni mikopo ya Kopafasta