Watumishi wa Serikali wamekumbushwa kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kazi ikiwemo uwajibikaji wa pamoja kwa mujibu wa taratibu zilizopo ili kuleta ufanisi katika ukamilishaji wa shughuli za maendeleo na kuwatumikia Wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa wakati wa Semina ya maadili kwa watumishi hao ya kuwakumbusha uzingatiaji wa taratibu katika utekelezaji wa majukumu na kuongeza kuwa ufanikishaji wa mambo hayo pia utafanikiwa iwapo watawajibika kama timu.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa.
Amesema, “uwajibikaji wa pamoja, lazima watumishi wwajibike kwa pamoja kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo lakini kutengeneza pia ‘team work’ ndani ya Halmashauri kuepuka migongano isiyo ya lazima ambayo inaweza kukwamisha shughuli za maendeleo.”
Awali Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Amina Nalicho alisema ujio wa teknolojia ambayo hubadilika kulingana na nyakati inasaidia kuwakumbusha majukumu yao kutokana na pia kuondoa usahaulifu wa Binadamu ambao ni kawaida katika maisha.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Amina Nalicho.
“Semina hii si mara ya kwanza lakini ni muhimu kukumbushana maana kama binadamu kuna usahaulifu lakini pia teknolojia inakuja kila wakati na watu wanafanya tafiti kuboresha hayo baadili kwahiyo tupo hapa ili kusisitizana uzingatiaji wa maadili ya uongozi,” amesema Bi. Nalicho.
Kwa upande wake Afisa Elimu Shule za Msingi jiji la Mbeya, Anderson Mwalongo ameishukuru tume ya maadili kwa kuwaongezea maarifa katika utendaji wao wa kazi kwani utekelezaji wa kazi huendana na uvunjifu wa maadili hivyo ni muhimu kukumbushana mambo muhimu.
Afisa Elimu Shule za Msingi jiji la Mbeya, Anderson Mwalongo.
Amesema, “uwajibikaji wa pamoja wakati mwingine pia umekuwa na uvunjifu wa maadili kwa sisi tunaosimamia viongozi wa umma, mnakuwa na makubaliano ambayo yapo kisheria lakini baadhi ya watu hutoa siri za vikao sasa hii inakuwa tayari umekiuka.”