Waajiri nchini, wametakiwa kulipa asilimia tatu ya michango ya Bima ya afya kwa wakati, ili watumishi wapate haki zao za matibabu.
Wito huo umetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia maelfu ya wafanyakazi, waliojumuika pamoja kuadhimisha siku ya wafanyakazi ambayo kitaifa imefanyika Mkoani Morogoro.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema, “kuna suala la wale watumishi wanaochangia asilimia tatu lakini mwajiri hapeleki, hili nalo mkaliangalie ili waajiriwa wapate haki zao za matibabu, madai yote yalipwe ndani ya siku 60 kama kuna mtu alijilimbikizia ndani ya siku 60 alipe madai yote wafanyakazi wafaidike na bima zao za afya.”
Awali, Katibu wa Shirikisho la Wafanyakazi -TUCTA, Hery Mkunda alisema mwajiri anapochelewesha michango wa matibabu ya Bima ya afya, mtumishi hupata changamoto ya kukosa huduma wakati tayari akiwa ameshakatwa asilimia tatu.